40
Faraja Kwa Watu Wa Mungu
Wafarijini, wafarijini watu wangu,
asema Mungu wenu.
Sema na Yerusalemu kwa upole,
umtangazie
kwamba kazi yake ngumu imekamilika,
kwamba dhambi yake imefanyiwa fidia,
kwamba amepokea kutoka mkononi mwa Bwana
maradufu kwa ajili ya dhambi zake zote.
 
Sauti ya mtu aliaye:
“Itengenezeni jangwani njia ya Bwana,
nyoosheni njia kuu nyikani
kwa ajili ya Mungu wetu.
Kila bonde litainuliwa,
kila mlima na kilima kitashushwa;
penye mabonde patanyooshwa,
napo palipoparuza patasawazishwa.
Utukufu wa Bwana utafunuliwa,
nao wanadamu wote watauona pamoja.
Kwa maana kinywa cha Bwana kimenena.”
 
Sauti husema, “Piga kelele.”
Nami nikasema, “Nipige kelele gani?”
 
“Wanadamu wote ni kama majani,
nao utukufu wao wote
ni kama maua ya kondeni.
Majani hunyauka na maua huanguka,
kwa sababu pumzi ya Bwana huyapuliza.
Hakika wanadamu ni majani.
Majani hunyauka na maua huanguka,
lakini neno la Mungu wetu ladumu milele.”
 
Wewe uletaye habari njema Sayuni,
panda juu ya mlima mrefu.
Wewe uletaye habari njema Yerusalemu,
inua sauti yako kwa kupiga kelele,
inua sauti, usiogope;
iambie miji ya Yuda,
“Yuko hapa Mungu wenu!”
10 Tazameni, Bwana Mwenyezi anakuja na nguvu,
nao mkono wake ndio utawalao kwa ajili yake.
Tazameni, ujira wake u pamoja naye,
nayo malipo yake yanafuatana naye.
11 Huchunga kundi lake kama mchungaji wa mifugo:
Hukusanya wana-kondoo katika mikono yake
na kuwachukua karibu na moyo wake,
huwaongoza taratibu wale wanyonyeshao.
 
12 Ni nani aliyepima maji ya bahari
kwenye konzi ya mkono wake,
au kuzipima mbingu kwa shibiri* yake?
Ni nani aliyeyashika mavumbi ya dunia katika kikapu,
au kupima milima kwenye kipimio
na vilima kwenye mizani?
13 Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana,
au kumfundisha akiwa kama mshauri wake?
14 Ni nani ambaye Bwana ametaka shauri kwake ili kumwelimisha,
naye ni nani aliyemfundisha njia iliyo sawa?
Ni nani aliyemfundisha maarifa
au kumwonyesha mapito ya ufahamu?
 
15 Hakika mataifa ni kama tone ndani ya ndoo,
ni kama vumbi jembamba juu ya mizani,
huvipima visiwa kana kwamba vilikuwa vumbi laini.
16 Lebanoni hautoshi kwa moto wa madhabahuni,
wala wanyama wake hawatoshi kwa sadaka za kuteketezwa.
17 Mbele yake mataifa yote ni kama si kitu,
yanaonekana yasio na thamani
na zaidi ya bure kabisa.
 
18 Basi, utamlinganisha Mungu na nani?
Utamlinganisha na kitu gani?
19 Kwa habari ya sanamu, fundi huisubu,
naye mfua dhahabu huifunika kwa dhahabu
na kuitengenezea mikufu ya fedha.
20 Mtu aliye maskini sana asiyeweza kuleta sadaka kama hii
huuchagua mti usiooza.
Humtafuta fundi stadi
wa kusimamisha sanamu ambayo haitatikisika.
 
21 Je, hujui?
Je, hujasikia?
Je, hujaambiwa tangu mwanzo?
Je, hujafahamu tangu kuumbwa kwa dunia?
22 Anakaa kwenye kiti cha enzi juu ya duara ya dunia,
nao watu wakaao ndani yake ni kama panzi.
Huzitandaza mbingu kama chandarua,
na kuzitandaza kama hema la kuishi.
23 Huwafanya wakuu kuwa si kitu,
na kuwashusha watawala wa dunia hii kuwa kitu bure.
24 Mara baada ya kupandwa,
mara baada ya kutiwa ardhini,
mara baada ya kutoa mizizi yao ardhini,
ndipo huwapulizia nao wakanyauka,
nao upepo wa kisulisuli
huwapeperusha kama makapi.
 
25 “Utanilinganisha mimi na nani?
Au ni nani anayelingana nami?” asema yeye Aliye Mtakatifu.
26 Inueni macho yenu mtazame mbinguni:
Ni nani aliyeumba hivi vyote?
Ni yeye aletaye nje jeshi la nyota moja baada ya nyingine
na kuziita kila moja kwa jina lake.
Kwa sababu ya uweza wake mkuu na nguvu zake kuu,
hakuna hata mojawapo inayokosekana.
 
27 Kwa nini unasema, ee Yakobo,
nanyi ee Israeli, kulalamika,
“Njia yangu imefichwa Bwana asiione,
Mungu wangu hajali shauri langu?”
28 Je wewe, hufahamu?
Je wewe, hujasikia?
Bwana ni Mungu wa milele,
Muumba wa miisho ya dunia.
Hatachoka wala kulegea,
wala hakuna hata mmoja
awezaye kuupima ufahamu wake.
29 Huwapa nguvu waliolegea
na huongeza nguvu za wadhaifu.
30 Hata vijana huchoka na kulegea,
nao vijana wanaume hujikwaa na kuanguka,
31 bali wale wamtumainio Bwana
atafanya upya nguvu zao.
Watapaa juu kwa mbawa kama tai;
watapiga mbio wala hawatachoka,
watatembea kwa miguu wala hawatazimia.
* 40:12 Shibiri ni sawa na sentimita 20 au inchi 8.