10
Israeli alikuwa mzabibu uliostawi sana,
alijizalia matunda mwenyewe.
Kadiri matunda yake yalivyoongezeka,
alijenga madhabahu zaidi;
kadiri nchi yake ilivyostawi,
alipamba mawe yake ya ibada.
Moyo wao ni mdanganyifu,
nao sasa lazima wachukue hatia yao.
Bwana atabomoa madhabahu zao
na kuharibu mawe yao ya ibada.
 
Kisha watasema, “Hatuna mfalme
kwa sababu hatukumheshimu Bwana.
Lakini hata kama tungelikuwa na mfalme,
angeweza kutufanyia nini?”
Wanaweka ahadi nyingi,
huapa viapo vya uongo
wanapofanya mapatano;
kwa hiyo mashtaka huchipuka
kama magugu ya sumu
katika shamba lililolimwa.
Watu wanaoishi Samaria huogopa
kwa ajili ya sanamu ya ndama ya Beth-Aveni.*
Watu wake wataiombolezea,
vivyo hivyo kuhani wake wa kuabudu sanamu,
wale waliokuwa wamefurahia fahari yake,
kwa sababu itaondolewa kutoka kwao
kwenda uhamishoni.
Itachukuliwa kwenda Ashuru
kama ushuru kwa mfalme mkuu.
Efraimu atafedheheshwa;
Israeli ataaibika kwa ajili ya sanamu zake za mti.
Samaria na mfalme wake wataelea
kama kijiti juu ya uso wa maji.
Mahali pa kuabudia sanamu pa uovu pataharibiwa:
ndiyo dhambi ya Israeli.
Miiba na mibaruti itaota
na kufunika madhabahu zao.
Kisha wataiambia milima, “Tufunikeni!”
na vilima, “Tuangukieni!”
 
“Tangu siku za Gibea, mmetenda dhambi, ee Israeli,
huko ndiko mlikobaki.
Je, vita havikuwapata
watenda mabaya huko Gibea?
10 Wakati nitakapopenda, nitawaadhibu;
mataifa yatakusanywa dhidi yao
ili kuwaweka katika vifungo
kwa ajili ya dhambi zao mbili.
11 Efraimu ni mtamba wa ngʼombe aliyefundishwa
ambaye hupenda kupura,
hivyo nitamfunga nira
juu ya shingo yake nzuri.
Nitamwendesha Efraimu,
Yuda lazima alime,
naye Yakobo lazima avunjavunje
mabonge ya udongo.
12 Jipandieni wenyewe haki,
vuneni matunda ya upendo usio na kikomo,
vunjeni ardhi yenu isiyolimwa;
kwa kuwa ni wakati wa kumtafuta Bwana,
mpaka atakapokuja
na kuwanyeshea juu yenu haki.
13 Lakini mmepanda uovu,
mkavuna ubaya,
mmekula tunda la udanganyifu.
Kwa sababu mmetegemea nguvu zenu wenyewe
na wingi wa mashujaa wenu,
14 mngurumo wa vita utainuka dhidi ya watu wako,
ili kwamba ngome zako zote zitaharibiwa:
kama Shalmani alivyoharibu Beth-Arbeli katika siku ile ya vita,
wakati mama pamoja na watoto wao
walipotupwa kwa nguvu ardhini.
15 Ndivyo itakavyotokea kwako, ee Betheli,
kwa sababu uovu wako ni mkuu.
Siku ile itakapopambazuka,
mfalme wa Israeli ataharibiwa kabisa.
* 10:5 Beth-Aveni maana yake Nyumba ya Ubatili (au Uovu), jina lingine la Betheli kwa dhihaka. 10:8 Yaani Aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni, jina lingine la Betheli kwa dhihaka.