8
Mwisho Wa Gharika
Mungu akamkumbuka Noa na wanyama wote wa porini na wa kufugwa waliokuwa naye ndani ya safina, akatuma upepo ukavuma katika dunia, nayo maji yakaondoka. Zile chemchemi zilizo chini sana ya ardhi pamoja na malango ya mafuriko ya mbinguni yakawa yamefungwa nayo mvua ikawa imekoma kunyesha kutoka angani. Maji yakaendelea kupungua taratibu katika nchi. Kunako mwisho wa siku ya 150, maji yalikuwa yamepungua, katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa saba, safina ikatua katika milima ya Ararati. Maji yakaendelea kupungua hadi mwezi wa kumi, na siku ya kwanza ya mwezi wa kumi, vilele vya milima vikaonekana.
Baada ya siku arobaini Noa akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina na akamtoa kunguru, akawa akiruka kwenda na kurudi mpaka maji yalipokwisha kukauka juu ya nchi. Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya uso wa ardhi. Lakini hua hakupata mahali pa kutua kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Noa ndani ya safina. Noa akanyoosha mkono akamchukua yule hua akamrudisha ndani ya safina. 10 Noa akangojea siku saba zaidi kisha akamtoa tena hua kutoka safina. 11 Wakati hua aliporejea kwa Noa jioni, alikuwa amechukua katika mdomo wake jani bichi la mzeituni, lililochumwa wakati ule ule! Ndipo Noa akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya uso wa dunia. 12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Noa.
13 Katika siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza ya mwaka 601, wa kuishi kwake Noa, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Noa akafungua mlango wa safina akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 14 Katika siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili dunia ilikuwa imekauka kabisa.
15 Ndipo Mungu akamwambia Noa, 16 “Toka ndani ya safina, wewe na mkeo na wanao na wake zao. 17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe: Ndege, wanyama na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
18 Kwa hiyo Noa akatoka nje pamoja na mkewe, wanawe na wake zao. 19 Wanyama wote na viumbe vyote vitambaavyo juu ya ardhi na ndege wote, kila kitu kiendacho juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina, kila aina ya kiumbe, kimoja baada ya kingine.
Noa Atoa Dhabihu
20 Kisha Noa akamjengea Bwana madhabahu, akachukua baadhi ya wale wanyama na ndege wote walio safi, akatoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. 21  Bwana akasikia harufu nzuri ya kupendeza, naye akasema moyoni mwake, “Kamwe sitailaani tena ardhi kwa sababu ya mwanadamu, hata ingawa kila mwelekeo wa moyo wake ni mbaya tangu ujana. Kamwe sitaangamiza tena viumbe hai vyote kama nilivyofanya.
22 “Kwa muda dunia idumupo,
wakati wa kupanda na wa kuvuna,
wakati wa baridi na wa joto,
wakati wa kiangazi na wa masika,
usiku na mchana
kamwe havitakoma.”