4
Kaini Na Abeli
Adamu akakutana kimwili na mkewe Eva, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Eva akasema, “Kwa msaada wa Bwana nimemzaa mwanaume.” Baadaye akamzaa Abeli ndugu yake.
Basi Abeli akawa mfugaji, na Kaini akawa mkulima. Baada ya muda Kaini akaleta baadhi ya mazao ya shamba kama sadaka kwa Bwana. Lakini Abeli akaleta fungu nono kutoka baadhi ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo yake. Bwana akamkubali Abeli pamoja na sadaka yake, lakini Mungu hakumkubali Kaini pamoja na sadaka yake. Kwa hiyo Kaini akakasirika sana, uso wake ukawa na huzuni.
Kisha Bwana akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika? Kwa nini uso wako una huzuni? Ukifanya lililo sawa, je, hutakubalika? Lakini usipofanya lililo sawa, dhambi inakuvizia mlangoni mwako, inakutamani wewe, lakini inakupasa uishinde.”
Basi Kaini akamwambia ndugu yake Abeli, “Twende shambani.” Walipokuwa shambani, Kaini akamshambulia Abeli ndugu yake, akamuua.
Kisha Bwana akamuuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”
Akamjibu, “Sijui, je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?”
10  Bwana akasema, “Umefanya nini? Sikiliza! Damu ya ndugu yako inanililia mimi kutoka ardhini. 11 Sasa umelaaniwa na umehamishwa kutoka ardhi, ambayo imefungua kinywa chake na kupokea damu ya ndugu yako kutoka mkononi mwako. 12 Utakapoilima ardhi, haitakupa tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga duniani asiye na utulivu.”
13 Kaini akamwambia Bwana, “Adhabu yangu ni zaidi ya niwezavyo kustahimili. 14 Leo unanifukuza kutoka nchi, nami nitafichwa mbali na uwepo wako. Nitakuwa mtu wa kutangatanga asiyetulia duniani na yeyote anionaye ataniua.”
15 Lakini Bwana akamwambia, “La sivyo, ikiwa mtu yeyote atamuua Kaini atalipizwa kisasi mara saba zaidi.” Kisha Bwana akamwekea Kaini alama ili mtu yeyote ambaye angemwona asimuue. 16 Kwa hiyo Kaini akaondoka mbele za Bwana akaenda kuishi katika nchi ya Nodi, iliyoko mashariki ya Edeni.
17 Kaini akakutana kimwili na mkewe, naye akapata mimba na akamzaa Enoki. Wakati huo Kaini alikuwa anajenga mji, akauita Enoki jina la mtoto wake. 18 Enoki akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli, Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, na Methushaeli akamzaa Lameki.
19 Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada, na mwingine Sila. 20 Ada akamzaa Yabali ambaye ni baba wa wale walioishi katika mahema na kufuga wanyama. 21 Kaka yake aliitwa Yubali, aliyekuwa baba wa wote wapigao zeze na filimbi. 22 Pia Sila alikuwa na mtoto wa kiume aliyeitwa Tubali-Kaini ambaye alifua vifaa vya aina mbalimbali vya shaba na chuma. Naama alikuwa dada wa Tubali-Kaini.
23 Lameki akawaambia wake zake,
“Ada na Sila nisikilizeni mimi;
wake wa Lameki sikieni maneno yangu.
Nimemuua mtu kwa kunijeruhi,
kijana mdogo kwa kuniumiza.
24 Kama Kaini atalipizwa kisasi mara saba,
basi Lameki itakuwa mara sabini na saba.”
25 Adamu akakutana kimwili na mke wake tena, akamzaa mwana, akamwita Sethi, akisema, “Mungu amenijalia mwana mwingine badala ya Abeli, kwa kuwa Kaini alimuua.” 26 Naye Sethi akamzaa mwana, akamwita Enoshi.
Wakati huo watu wakaanza kuliitia jina la Bwana.