32
Yakobo Ajiandaa Kukutana Na Esau
Yakobo pia akaondoka akaenda zake, nao malaika wa Mungu wakakutana naye. Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.*
Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu. Akawaagiza akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema, nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwako huko mpaka sasa. Ninao ngʼombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”
Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulikwenda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume 400.”
Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili, pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vilevile ngʼombe na ngamia. Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litaweza likanusurika.”
Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaki, Ee Bwana, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’ 10 mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili. 11 Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia mama pamoja na watoto wao. 12 Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”
13 Akalala pale usiku ule, miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake: 14 Mbuzi waume ishirini na mbuzi wake 200, kondoo dume ishirini na kondoo wake 200. 15 Ngamia wake thelathini pamoja na ndama zao, ngʼombe wake arobaini na mafahali kumi, punda wake ishirini na punda waume kumi. 16 Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”
17 Akamwagiza yule aliyetangulia kuwa, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’ 18 Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”
19 Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye. 20 Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.” 21 Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.
Yakobo Ashindana Mweleka Na Mungu
22 Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki. 23 Baada ya kuwavusha ngʼambo ya kijito, alivusha pia mali zake zote. 24 Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake na mtu mmoja akashikana naye mweleka mpaka mapambazuko. 25 Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo kwa hiyo nyonga yake ikateguka wakati alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu. 26 Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.”
Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”
27 Yule mtu akamuuliza, “Jina lako nani?”
Akajibu, “Yakobo.”
28 Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”
29 Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.”
Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.
30 Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akasema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso na bado maisha yangu yameokoka.”
31 Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake. 32 Kwa hiyo mpaka leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.
* 32:2 Mahanaimu maana yake Kambi mbili. 32:28 Israeli maana yake Yeye ashindanaye na Mungu. 32:30 Penieli maana yake Uso wa Mungu, ambalo ni sawa na Penueli kwa Kiebrania.