25
Kifo Cha Abrahamu
Abrahamu alioa mke mwingine, ambaye jina lake aliitwa Ketura. Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani, wazao wa Dedani walikuwa Waashuri, Waletushi na Waleumi. Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.
Abrahamu akamwachia Isaki kila kitu alichokuwa nacho. Lakini Abrahamu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaki.
Kwa jumla, Abrahamu aliishi miaka 175. Ndipo Abrahamu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake. Watoto wake Isaki na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti, 10 Shamba ambalo Abrahamu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Abrahamu alipozikwa pamoja na mkewe Sara. 11 Baada ya kifo cha Abrahamu, Mungu akambariki mwanawe Isaki, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.
Wana Wa Ishmaeli
12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mtoto wa Abrahamu, ambaye mjakazi wake Sara, Hagari Mmisri, alimzalia Abrahamu.
 
13 Haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, yaliyoorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi, akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu, 14 Mishma, Duma, Masa, 15 Hadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema. 16 Hawa walikuwa wana wa Ishmaeli na haya ni majina ya viongozi wa makabila kumi na mawili kulingana na makao yao na kambi zao. 17 Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka 137. Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake. 18 Wazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, unapoelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.
Yakobo Na Esau
19 Hivi ndivyo vizazi vya Isaki mwana wa Abrahamu.
 
Abrahamu akamzaa Isaki, 20 Isaki alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.
21 Isaki akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Bwana akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. 22 Watoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Bwana.
23  Bwana akamjibu,
“Mataifa mawili yamo tumboni mwako,
na mataifa hayo mawili
kutoka ndani yako watatenganishwa.
Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine,
na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
24 Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. 25 Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau.* 26 Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo. Isaki alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa.
27 Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. 28 Isaki, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.
29 Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. 30 Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.)
31 Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
32 Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”
33 Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa.
34 Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake.
Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
* 25:25 Esau maana yake Mwenye nywele nyingi. 25:26 Yakobo maana yake Ashikaye kisigino, au Atwaaye mahali pa mwingine, au Mdanganyaji, au Mwenye hila, au Mlaghai, au Mjanja. 25:30 Edomu maana yake Mwekundu.