20
Amri Kumi
(Kumbukumbu 5:1-21)
1 Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:
2 “Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
3 Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4 Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji.
5 Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
6 lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
7 Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
8 Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase.
9 Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote,
10 lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
11 Kwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
12 Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.
13 Usiue.
14 Usizini.
15 Usiibe.
16 Usimshuhudie jirani yako uongo.
17 Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”
Watu Wanaogopa
(Kumbukumbu 5:22-33)
18 Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali
19 na wakamwambia Mose, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”
20 Mose akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”
21 Watu wakabaki mbali, wakati Mose alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.
Sanamu Na Madhabahu
22 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni:
23 Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.
24 “ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo zako, mbuzi na ngʼombe zako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki.
25 Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi.
26 Msitumie ngazi kupandia kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’