16
Mana Na Kware
Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri. Huko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni. Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa Bwana huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”
Kisha Bwana akamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu. Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”
Kwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwamba Bwana ndiye aliwatoa Misri, kisha asubuhi mtauona utukufu wa Bwana, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?” Pia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Bwana wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya Bwana.”
Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Bwana, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ”
10 Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Bwana ukitokeza katika wingu.
11 Bwana akamwambia Mose, 12 “Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”
13 Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi. 14 Wakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa. 15 Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.
Mose akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Bwana amewapa mle. 16 Hivi ndivyo Bwana alivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi* moja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ”
17 Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu. 18 Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.
19 Kisha Mose akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote mpaka asubuhi.”
20 Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia.
21 Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka. 22 Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Mose. 23 Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”
24 Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu. 25 Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana. Hamtapata chochote juu ya nchi leo. 26 Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.”
27 Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote. 28 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini? 29 Fahamuni kuwa Bwana amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.” 30 Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.
31 Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali. 32 Mose akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”
33 Kwa hiyo Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Bwana ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”
34 Kama Bwana alivyomwagiza Mose, hatimaye Aroni alikuja kuihifadhi ndani ya Sanduku la Ushuhuda. 35 Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.
36 (Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.)
* 16:16 Pishi ni kipimo cha ujazo, kwa Kiebrania ni omeri, ambacho ni sawa na kilo mbili. 16:31 Mana maana yake ni mkate kutoka mbinguni. 16:36 Efa moja ni sawa na kilo 22.