48
Mgawanyo Wa Nchi
“Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kwenye mpaka wa kaskazini, Dani atakuwa na sehemu moja, mpaka huo utafuata barabara ya Hethloni hadi Lebo-Hamathi, Hasar-Enani hata mpaka wa kaskazini wa Dameski karibu na Hamathi utakuwa sehemu ya huo mpaka wake kuanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
“Asheri atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Dani kuanzia mashariki hadi upande wa magharibi.
“Naftali atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Asheri kuanzia mashariki hadi magharibi.
“Manase atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Naftali kuanzia mashariki hadi magharibi.
“Efraimu atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Manase kuanzia mashariki hadi magharibi.
“Reubeni atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Efraimu kuanzia mashariki hadi magharibi.
“Yuda atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Reubeni kuanzia mashariki hadi magharibi.
“Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa 25,000* na urefu wake kuanzia mashariki mpaka magharibi utakuwa ule ule wa sehemu moja ya kabila, mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo.
“Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwa Bwana itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000 10 Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kaskazini, upana wa dhiraa 10,000 upande wa magharibi, dhiraa 10,000 upande wa mashariki na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu pa Bwana. 11 Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka. 12 Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani, sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi.
13 “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. 14 Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa Bwana.
15 “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa 5,000 na urefu wa dhiraa 25,000, litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na malisho. Mji utakuwa katikati yake 16 nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa 4,500,§ upande wa kusini dhiraa 4,500, upande wa mashariki dhiraa 4,500 na upande wa magharibi dhiraa 4,500. 17 Sehemu ya malisho kwa ajili ya mji itakuwa na eneo la dhiraa 250* upande wa kaskazini, dhiraa 250 upande wa kusini, dhiraa 250 upande wa mashariki na dhiraa 250 upande wa magharibi. 18 Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa 10,000 upande wa mashariki na dhiraa 10,000 upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula. 19 Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli. 20 Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani, dhiraa 25,000 kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji.
21 “Eneo linalobaki pande zote za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu atawalaye. Eneo hili litaenea upande wa mashariki kuanzia kwenye dhiraa 25,000 za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki na kuelekea upande wa magharibi kuanzia kwenye dhiraa 25,000 hadi mpaka wa magharibi. Maeneo yote haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake. 22 Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini.
23 “Kuhusu makabila yaliyobaki: Benyamini atakuwa na sehemu moja, itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
24 “Simeoni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi.
25 “Isakari atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi.
26 “Zabuloni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi.
27 “Gadi atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi.
28 “Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu.
29 “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asema Bwana Mwenyezi.
Malango Ya Mji
30 “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu, 31 malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.
32 “Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani.
33 “Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni.
34 “Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.
35 “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa 18,000.
“Nalo jina la mji huo kuanzia wakati huo na kuendelea litakuwa:
 
Bwana yupo hapa.”
* 48:8 Dhiraa 25,000 ni sawa na kilomita 11.25. 48:9 Dhiraa 10,000 ni sawa na kilomita 4.5. 48:15 Dhiraa 5,000 ni sawa na kilomita 2.25. § 48:16 Dhiraa 4,500 ni sawa na kilomita 2.025. * 48:17 Dhiraa 250 ni sawa na sentimita 112.5. 48:28 Bahari Kuu hapa ina maana ya Bahari ya Mediterania. 48:35 Dhiraa 18,000 ni sawa na kilomita 8.1.