44
Mkuu, Walawi, Makuhani
1 Ndipo yule mtu akanirudisha mpaka kwenye lango la nje la mahali Patakatifu, lile linaloelekea upande wa mashariki, nalo lilikuwa limefungwa.
2 Bwana akaniambia, “Lango hili litabaki limefungwa. Haliruhusiwi kufunguliwa, wala hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingilia kwenye lango hili. Litabaki limefungwa kwa sababu Bwana, Mungu wa Israeli, ameingia kwa kupitia lango hili.
3 Yeye aliye mkuu peke yake ndiye anayeweza kukaa penye njia ya hilo lango na kula chakula mbele za Bwana. Itampasa aingie kwa njia hiyo ya lango la ukumbini na kutokea njia iyo hiyo.”
4 Kisha yule mtu akanileta kwa njia ya lango la kaskazini mpaka mbele ya Hekalu. Nikatazama nami nikauona utukufu wa Bwana ukilijaza Hekalu la Bwana, nami nikaanguka kifudifudi.
5 Bwana akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa uangalifu, usikilize kwa bidii na uzingatie kila kitu ninachokuambia kuhusu masharti yote yanayohusu Hekalu la Bwana. Uwe mwangalifu kuhusu wale wanaoruhusiwa hekaluni na wale wasioruhusiwa kuingia mahali patakatifu.
6 Iambie nyumba ya kuasi ya Israeli, ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Matendo yenu ya machukizo yatosha, ee nyumba ya Israeli!
7 Zaidi ya matendo yenu yote ya machukizo, mmewaleta wageni wasiotahiriwa mioyo na miili katika patakatifu pangu, mkilinajisi Hekalu langu, huku mkinitolea chakula, mafuta ya wanyama na damu, nanyi mmevunja Agano langu.
8 Badala ya kutimiza wajibu wenu kuhusiana na vitu vyangu vitakatifu, mmeweka watu wengine kuwa viongozi katika patakatifu pangu.
9 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Hakuna mgeni asiyetahiriwa moyo na mwilini anayeruhusiwa kuingia patakatifu pangu, wala hata wageni wanaoishi miongoni mwa Waisraeli.
10 “ ‘Walawi walioniacha wakati Waisraeli walipopotoka wakatoka kwangu na kutangatanga kwa kufuata sanamu zao, watachukua adhabu ya dhambi zao.
11 Wanaweza wakatumika katika mahali patakatifu pangu, wakiwa na uangalizi wa malango ya Hekalu, nao watachinja sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa ajili ya watu na kusimama mbele ya watu ili kuwahudumia.
12 Lakini kwa sababu waliwatumikia watu mbele ya sanamu zao na kuifanya nyumba ya Israeli ianguke kwenye dhambi, kwa hiyo nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba ni lazima wachukue matokeo ya dhambi yao, asema Bwana Mwenyezi.
13 Hawaruhusiwi kukaribia ili kunitumikia kama makuhani wala kukaribia chochote changu kilicho kitakatifu au sadaka iliyo takatifu kupita zote, bali watachukua aibu ya matendo yao ya kuchukiza.
14 Lakini nitawaweka katika uangalizi wa Hekalu na kazi zote zile zinazotakiwa kufanyika ndani yake.
15 “ ‘Lakini makuhani, ambao ni Walawi na wazao wa Sadoki, ambao walitimiza wajibu wao kwa uaminifu katika patakatifu pangu wakati Waisraeli walipopotoka, watakaribia ili kutumika mbele zangu. Itawapasa wasimame mbele zangu ili kutoa dhabihu za mafuta ya wanyama na damu, asema Bwana Mwenyezi.
16 Wao peke yao ndio wenye ruhusa ya kuingia mahali patakatifu pangu. Wao peke yao ndio watakaokaribia meza yangu ili kuhudumu mbele zangu na kufanya utumishi wangu.
17 “ ‘Watakapoingia kwenye malango ya ukumbi wa ndani, watavaa nguo za kitani safi, hawaruhusiwi kamwe kuvaa mavazi ya sufu wakati wanapokuwa wakihudumu kwenye malango ya ukumbi wa ndani wala ndani ya Hekalu.
18 Watavaa vilemba vya kitani safi vichwani mwao na nguo za ndani za kitani safi viunoni mwao. Hawatavaa chochote kitakachowafanya kutoa jasho.
19 Watakapotoka ili kuingia katika ukumbi wa nje mahali watu walipo, watavua nguo walizokuwa wakihudumu nazo na wataziacha katika vyumba vitakatifu nao watavaa nguo nyingine, ili kwamba wasije wakaambukiza watu utakatifu kwa njia ya mavazi yao.
20 “ ‘Hawatanyoa nywele za vichwa vyao wala kuziacha ziwe ndefu, bali watazipunguza.
21 Kuhani yeyote asinywe mvinyo aingiapo katika ukumbi wa ndani.
22 Wasioe wanawake wajane wala walioachika, inawapasa kuoa wanawake bikira wenye heshima wa Israeli au wajane wa makuhani.
23 Watawafundisha watu wangu tofauti kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida na kuwaonyesha jinsi ya kupambanua kati ya vitu najisi na vitu safi.
24 “ ‘Katika magombano yoyote, makuhani watatumika kama mahakimu na kuamua hilo jambo kufuatana na sheria zangu. Watazishika sheria zangu na maagizo yangu katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa, nao watatakasa Sabato zangu.
25 “ ‘Kuhani asijitie unajisi kwa kukaribia maiti, lakini, kama mtu aliyekufa alikuwa baba yake au mama yake, mwana au binti yake, ndugu yake au dada ambaye hajaolewa, basi aweza kujitia unajisi kwa hao.
26 Baada ya kujitakasa, atakaa hali hiyo kwa muda wa siku saba.
27 Siku atakapoingia katika ukumbi wa ndani wa mahali patakatifu ili kuhudumu, atatoa sadaka ya dhambi kwa ajili yake mwenyewe, asema Bwana Mwenyezi.
28 “ ‘Mimi nitakuwa ndio urithi pekee walio nao makuhani katika Israeli. Msiwape wao milki, mimi nitakuwa milki yao.
29 Wao watakula sadaka za nafaka, sadaka za dhambi na sadaka za hatia na kila kitu kitakachotolewa kwa Bwana katika Israeli kitakuwa chao.
30 Yote yaliyo bora ya malimbuko ya vitu vyote na matoleo yenu maalum vitakuwa vya makuhani. Inawapasa kuwapa malimbuko ya kwanza ya unga wenu ili kwamba baraka ipate kuwa katika nyumba zenu.
31 Makuhani hawaruhusiwi kula chochote, ikiwa ni ndege au mnyama, aliyekutwa akiwa amekufa au aliyeraruliwa na wanyama pori.